Thursday, 26 June 2014

UCHAGUZI SIMBA: Rage aitwa Mahakamani




Mwenyekiti wa Klabu ya Simba anayemaliza muda wake, Ismail Aden Rage. 
Na Vicky Kimaro, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Juni26  2014  saa 12:32 PM
KWA UFUPI
Mahakama Kuu imemtaka Rage na Baraza la wadhamini kufika mahakamani hapo leo saa 3:00 asubuhi baada ya wanachama kufungua kesi kupinga uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Juni 29.
Dar es Salaam. Wakati Mahakama Kuu ikimuita mahakamani mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na baraza lake la wadhamani, wagombea uongozi wa klabu hiyo jana walizindua kampeni zao, huku suala uwanja wake na rasilimali watu likichukua nafasi kubwa.
Mahakama Kuu imemtaka Rage na Baraza la wadhamini kufika mahakamani hapo leo saa 3:00 asubuhi baada ya wanachama kufungua kesi kupinga uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Juni 29.
Wakili Revocatus Kuuli, ambaye anawawakilisha wanachama hao 69 waliofungua kesi na kuomba amri ya kusimamisha uchaguzi huo, alisema leo ndio kesi ya msingi itapangiwa tarehe ya kusikilizwa ikiwa ni pamoja na ombi lao la msingi la kutaka uchaguzi usimame kujulikana.
“Rage na baraza lake la wadhamini wamepelekewa wito wa kuitwa mahakamani kesho (leo) saa 3:00 asubuhi. Sasa kufika au kutofika hiyo ni juu yao. Sisi tunasubiri majibu ya ombi letu ambalo ni kuzuia uchaguzi hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa,” alisema Kuuli.
Hadi jana jioni, Rage alikuwa mjini Dodoma ambako anashiriki kwenye Bunge la Bajeti na alichangia hoja majira ya saa 12:15.
Wanachama 69 wanaowakilishwa na Hassan Abdallah, Josephat Waryoba na Said Ally, walifungua kesi wakitaka izuie kufanyika uchaguzi huo kwa kile walichodai kuwa katiba imekiukwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba haijaundwa kikatiba.
Pia, wanachama hao wa Simba wanalalamikia kutokuwapo kwa Kamati ya Maadili iliyotakiwa kuundwa kwa ajili ya kusikiliza masuala mengi yahusuyo maadili ambayo hadi sasa hayajatatuliwa.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, katibu mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema:
“Sijui lolote... sina taarifa kama kuna wito ambao umetolewa na mahakama. Sikuwapo ofisini, labda kama taarifa hiyo ilipelekwa ofisini.”
Hata hivyo, wakati mahakama ikitoa wito huo, mgombea wa nafasi ya urais, Evans Aveva alisema atampa muda wa kujitathmini kocha wa timu hiyo, Zradvko Logarusic kabla ya kutoa nafasi zaidi kwa makocha wazawa.
“Nitawapa kipaumbele makocha wazalendo, lakini kwanza sina budi kutoa nafasi kwa Loga. Tutaangalia uwezo wake na matakwa yetu kisha tutaamua,” alisema.
Aveva alisema Simba, ambayo ina miaka 78 tangu kuanzishwa kwake, hailingani na hadhi yake kwa kuwa imeshindwa kujiendesha kiuchumi na kumiliki uwanja. “Kwa sasa Simba ina wanachama 7,000 nitajitaidi ndani ya miaka minne wafikie 50,000 ili kuitoa Simba hapa ilipo.”

No comments:

Post a Comment