MECHI ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Yanga na Al Ahly kutoka Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, imeingiza Sh448.4 milioni.
Mapato hayo yametokana na watazamaji 50,202 waliokata tiketi kuingia uwanjani kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya Sh7,000, Sh13,000, Sh25,000 na Sh 35,000. Yanga ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0.
Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni Sh68,402,135.59, gharama za kuchapa tiketi ni Sh10,343,219, waamuzi na kamishna Sh14,665,930 na matangazo Sh15,679,000.
Uwanja Sh50,898,557.31, gharama za mchezo Sh33,932,371.54, TFF na CAF Sh33,932,371.54 wakati Yanga ilipata mgawo wa Sh220,560,415.01.
Nayo mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa juzi Jumapili iliingiza Sh20,610,000 ambapo kila klabu ilipata mgawo wa Sh4,402,492 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni Sh3,143,898.31.
Katika hatua nyingine, mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Mlale JKT na Lipuli iliyokuwa ichezwe Jumapili katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, sasa imewahishwa na itachezwa kesho Jumatano.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko hayo ili kuipunguzia gharama Lipuli ya Iringa ambayo Jumapili ilicheza mechi mjini Songea dhidi ya Majimaji.
No comments:
Post a Comment